WATU 100 KUFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KOSA LA KUJIANDIKISHA MARA MBILI
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema inakusudia kuwafikisha mahakamani wananchi zaidi ya 100 wa Mkoa wa Njombe kwa madai ya kujiandikisha zaidi ya mara moja kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Naibu Katibu wa Tume hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Daftari na Tehama, Dk Sisti Cariah alisema wananchi hao wamebainika kwa kutumia teknolojia ya BVR na uhakiki huo utaendelea katika maeneo yote nchini.
Alisema picha na majina ya watuhumiwa hao vimepelekwa kwenye idara zinazohusika huku akiwaonya wananchi ambao hawajaandikishwa kuacha kudhani kwamba wanaweza kujiandikisha zaidi ya mara moja bila kubainika.
“Kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa la jinai, unaweza ukafungwa, ukatozwa faini au vyote viwili kwa pamoja... hivi karibuni tutaanza kutoa picha zao na kuwatangaza kwenye vyombo vya habari waliojiandikisha mara mbili,” alisema Dk Cariah.
Mikoa iliyokamilisha uandikishaji
Akizungumzia mchakato wa uandikishaji, Dk Cariah alisema NEC imeshakamilisha uandikishaji katika mikoa mitano ambayo ni Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa na Njombe na hadi kufikia Juni 18 itakuwa imekamilisha uandikishaji kwenye mikoa mingine minane.
Kumekuwapo na mjadala mkubwa baada ya kubainika kuwa watu wamekuwa wakijiandikisha zaidi ya mara moja katika vituo tofauti na kuibua hofu ya uchakachuaji kufanyika katika Uchaguzi Mkuu.
Yaahirisha mikoa mitano
Katika hatua nyingine NEC imesogeza mbele uandikishaji wapigakura kwenye mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga na Morogoro kutokana na marekebisho ya mipaka ya kiutawala ya kata, mitaa, vijiji na vitongoji yaliyofanywa na Tamisemi.
Mikoa hiyo ambayo ilipaswa kuanza kuandikisha wapigakura kuanzia leo, sasa itaanza shughuli hiyo Juni 16. Alisema katika mikoa ya Geita, Mwanza na Simiyu uandikishaji utaanza leo kama ilivyopangwa na hakutakuwa na mabadiliko huku Mkoa wa Pwani uandikishaji ukitarajiwa kuanza Juni 20.
Kuhusu tathmini katika mikoa ambayo uandikishaji umeshafanyika, alisema Tume imevuka malengo kwa kuandikisha wananchi wengi kuliko hata idadi iliyokadiriwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). “Lengo la Tume ni kuandikisha watu milioni 21 nchi nzima lakini tunaweza kuandikisha watu milioni 24 ambao watakuwa na miaka 18 au zaidi,” alisema.
SOURCE: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment